Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo wa Tanzania Profesa Palamagamba Kabudi, amemuagiza Katibu Mkuu katika wizara yake kulishughulikia suala la kung’olewa kwa viti katika Dimba la Benjamin Mkapa tarehe 15 Disemba.
Taarifa kutoka kwa Msemaji Mkuu wa Serikali imethibitisha kuwa klabu ya Simba itatumiwa barua, huku nakala nyingine ikipelekwa kwa Shirikisho la Soka Tanzania, kuhakikisha kuwa gharama ya uharibifu huo inalipwa.
Vurugu zilitokea wakati wa mechi ya Kombe la Shirikisho barani Afrika kati ya Simba na CS Sfaxien, ambapo wenyeji Simba walipata ushindi wa magoli 2-1. Kulikuwa na hamaki na hisia kali katika mechi hiyo, hadi kufikia hatua ya kuharibu viti 256.
“Yaliyotokea jana katika dimba la Benjamin Mkapa hayakubaliki na ni kinyume na yanayotarajiwa katika michezo,” alisema Profesa Kabudi.
“Nimemuagiza Katibu Mkuu awaandikie barua klabu ya Simba na Shirikio la Soka Tanzania. Polisi pia wahakikishie wale wote waliohusika katika uharibifu huo wamekamatwa na hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao. Tabia hii lazima ikome.”
Waziri Kabudi pia alisisitiza umuhimu wa mashabiki kuheshimu maeneo ya viwanja vya michezo na kutojihusisha na uharibifu, akiwataka wazingatie mzigo wa kifedha utakaokabili serikali pamoja na kuharibu ubora wa kiwanja.
Kamanda wa Polisi Kanda maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, ameeleza kuwa vurugu zilitokea kufwatia ghadhabu za baadhi ya mashabiki wa CS Sfaxien ambapo walikuwa wamekasirishwa na maamuzi ya kuongezwa muda wa dakika saba baada ya dakika tisini, wakati ambapo timu ya Simba ilipata goli la ushindi.