Michezo

Kongamano la mpira wa Miguu Tanzania la zinduliwa Zanzibar

on

Kongamano la Mpira wa miguu Tanzania maarufu kama Tanzania Football Summit (TFS) kwa mwaka 2022 limezinduliwa rasmi leo katika hoteli ya Serena Zanzibar. Akizindua kongamano la mwaka 2022 ambalo linatarajiwa kufanyika Juni 25-26, 2022 visiwani Zanzibar, Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Lela Mohamed Mussa amesema lengo la Serikali zote mbili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ni kuboresha michezo na kutumia watu maarufu duniani ili kutangaza nchi kimataifa.

 

“Kufanyika kwa kongamano hili mwezi Juni hapa Zanzibar, tunatarajia kutatumia watu mbalimbali maarufu duniani ambao watakuwa chachu ya kutangaza utalii wa kimichezo nchini. Huu ni wakati mwafaka wa kutangaza vyakula vyetu vya hapa, nataka wakati wa kongamano wageni wetu wale vyakula vyetu vinavyotokana na bahari, wale samaki wa hapa kwetu”>>> Waziri Lela.

Waziri Mhe. Lela ameongeza kuwa kongamano la TFS limekuja muda mwafaka likiongozwa na kaulimbiu ya mwaka huu inayosema “Maendeleo ya Mpira wa Miguu kwa Uchumi wa Buluu” kuwa ni hatua ya kuunga mkono sera ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ya Awamu wa Nane chini ya Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Ali Mwinyi inayolenga katika matumizi endelevu ya rasimali za bahari katika kuleta maendeleo kwa wananchi wa Zanzibar.

Akipokea taarifa ya kongamano la mwaka 2021, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Tanzania bara Bw. Saidi Yakubu Yakubu amesema wataifanyia kazi taarifa hiyo na kuahidi kuyafanyia kazi maazimio ya mwaka jana na kuwapongeza waandaji wa kongamano kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi inayojali michezo katika kujenga uchumi na kuwapongeza Kamati maalumu ya inayoandaa kongamano la mwezi Juni 2022 ambapo tayari mada zake zimeandaliwa kwa wakati. Naibu Katibu Mkuu Yakubu amesema mchezo wa soka unafursa kubwa katika ujenzi wa uchumi wa taifa ambao unamchango mkubwa kwenye mapato ya Serikali kupitia kupitia ligi mbalimbali zinazoendeshwa nchini.

Ameongeza kuwa utalii wa kimichezo umekuwa kiungo muhimu katika nchi ambayo inalenga kuendesha michezo kisayansi na kusema Zanzibar maeneo mazuri ya kuwekeza kwenye sekta ya michezo yapo ikiwemo fukwe na bahari ambazo ni chanzo cha vivutio vya watalii.

Kwa upande wake Katibu wa Kamati ya Maalum ya Maandalizi ya kongamano hilo ambaye pia Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Afrisoccer inajishughulisha na shunghuli za Michezo Bw. Peter Simon amesema walengwa wakuu wa kongamano hilo ni wadau mbalimbali wa mpira ikiwemo Serikali, wasimamizi wa mpira wa Miguu ikiwemo Shirikisho la Mpira, vilabu, Makocha, wachezaji wa zamani, wawekezaji, makampuni binafsi, mawakala, waandishi wa habari na wapenzi na mashabiki wa mpira wa miguu. Ameongeza kuwa Kongamano hili lina malengo makuu matatu ikiwa ni pamoja na kutoa nafasi kwa wadau wa mpira wa miguu na kutoka katika sekta nyingine ndani na nje ya nchi kujadili na kutafuta ufumbuzi wa changamoto mbalimbali ili kuleta mabadiliko chanya katika mpira wa miguu na maendeleo kwa ujumla.

Lengo nyingine ni kwa wadau kufahamiana na kutengeneza fursa mbalimbali za kibiashara na lengo la tatu ni kutoa nafasi kwa wadau kujifunza na kubadilishana ujuzi na uzoefu kupitia mada mbalimbali zitakazowasilishwa na kujadiliwa na wazungumzaji wazoefu na wabobefu kutoka ndani na nje ya nchi.

Kongamano la mwaka huu linatarajiwa kuwa na mada sita ambazo zitajadiliwa ikiwemo Nafasi za Uwekezaji katika Mpira wa Miguu, Uongozi na Usimamizi wa Mpira wa Miguu, Utalii wa Michezo, Sheria za Michezo, Mpira wa Miguu katika janga la Uviko 19, Matumizi ya Mpira wa Miguu katika kutatua changamoto mbalimbali za Kijamii. na kusistiza maazimio yatakayotokana na majadiliano hayo yatawasilishwa katika ngazi mbalimbali za maamuzi ili kusaidia katika kutunga wa sera na miongozo mbalimbali.

Kongamano la kwanza lililofanyika mwaka jana jijini Dar es Salaam huku washiriki wake wakitoka mataifa zaidi ya kumi ikiwemo Ufaransa, Ubeligiji, Ujerumani, Afrika Kusini, Uganda, Misri, Israeli, Senegali na Cameroon na kutibu kiu na matarajio ya malengo ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambapo Uchumi wa Buluu umejikita kuwatumia pia watu maarufu duniani kutangaza fursa za kiuchumi zilizopo Visiwani humo.

Katika kongamano la mwaka huu linatarajiwa kuhudhuriwa kuwa na washiriki zaidi ya 500 kutoka ndani na nje ya nchi wakati mwaka 2021 kongamano hilo lilihudhuriwa na washiriki zaidi ya 150 na kuwavutia wachezaji magwiji wa soka waliotamba barani Afrika na duniani ambao pia wanatarajiwa kushiriki kongamano la mwaka huu ambao ni Khalilou Fadiga, mchezaji wa zamani wa timu ya taifa ya Senegal na vilabu mbalimbali vikiwemo PSG na Bolton Wanderers pamoja na nyota wa zamani wa timu ya taifa ya Cameroon Patrick Mboma ambaye pia alicheza katika vilabu kama vile PSG na Parma.

Uzinduzi wa leo umehudhuriwa pia na viongozi mbalimbali akiwemo Kamishna wa Michezo Zanzibar Ndugu Ameir Mohamed Makame, Rais wa Shirikisho la Mpira Zanzibar (ZFF) Abdul-Latif Ali Yasini, Mkurugenzi wa Uwekezaji Pemba Al-Haji Mtumwa Jecha, Mkurugenzi Mtendaji wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar Bi. Hafsa Mbamba na Mkurugenzi wa Uratibu na Maendeleo ya Uchumi wa Buluu Kapteni Hamad Bakar Hamad. Wengine waliohudhuria ni wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya TFS wakiongozwa na Mwenyekiti wa bodi hiyo Bi. Nassra Juma Mohamed ambaye pia ni Naibu Kamishna wa Uhamiaji Zanzibar na Makamu Mwenyekiti wa Bodi hiyo Dr. Tumaini M. Katunzi ambaye pia ni Mkuu wa Chuo cha Takwimu Mashariki ya Afrika.

Soma na hizi

Tupia Comments