Wachezaji wa Korea Kaskazini, Kim Kum-yong na Ri Jong-sik wanaripotiwa kuwekwa chini ya ‘uchunguzi wa kiitikadi’ na wanaweza kukabiliwa na adhabu ikiwa watashindwa kujitetea kutokana na tabia isiyofaa waliyoonyesha kwenye michezo ya Olimpiki mwaka huu.
Mojawapo ya picha zinazosherehekewa zaidi za katika michezo ya Olimpiki iliyomalizika huko Paris, Ufaransa ni “selfie” iliyopigwa na wachezaji wa tenisi ya mezani, walioshinda medali kutoka pande zote za peninsula ya Korea iliyogawanyika, picha hiyo inaonekana kuwaingiza matatizoni wachezaji hao baada ya kurejea nyumbani.
Kwa watazamaji wengi wa Olimpiki, ilikuwa ni uthibitisho wa uwezo wa michezo kuunganisha watu na kuwaleta pamoja licha ya changamoto za kimaisha na mipaka ya kinchi, lakini kwa Korea Kaskazini wameichukulia picha hiyo kama usaliti ulioonyeshwa na wachezaji wao kukubali kupiga picha na mahasimu wao.