Korea Kaskazini imelipua barabara za Korea Kusini ambazo zilikua hazitumiki tena katika eneo la kaskazini mwa Nchi hiyo leo Jumanne, October 15, 2024 Mamlaka za Korea Kusini zimethibitisha tukio hilo.
Chuki imeendelea kuongezeka maradufu baina ya Mataifa hayo mawili ya Korea mara baada ya Korea Kaskazini kuituhumu Korea Kusini kuwa ilirusha ndege zisizo na rubani kuelekea Mji Mkuu wa Nchi hiyo wa Pyongyang.
Ubomoaji wa barabara hizo unaonyesha namna Korea Kaskazini inaichukia Serikali ya kihafidhina ya Korea Kusini huku Kiongozi wake Kim Jong Un akiahidi kuvunja uhusiano na kuachana na lengo la kufikia umoja wa Korea kwa amani.
Waangalizi wa mambo wanasema bado kuna uwezekano kwamba Kim ataanzisha mashambulizi makubwa dhidi ya Korea Kusini kujaribu kutishia kikosi cha juu cha Korea Kusini-Marekani ambacho kinaweza kuwa tishio katika maisha yake.
Video iliyotolewa na Jeshi la Korea Kusini imeonyesha wingu la moshi mweupe na wa kijivu ukiibuka kutokana na mlipuko huo kwenye barabara karibu na Mji wa mpakani wa Kaesong na Korea Kaskazini, Jeshi hilo limesema linajiandaa kwa lolote.