Korea Kaskazini inashutumiwa kuwaadhibu hadharani Wasichana wadogo na Vijana wanaotizama tamthilia au televisheni zilizopigwa marufuku Nchini humo ikiwemo televisheni za Korea Kusini, China na Mataifa ya Magharibi.
Video mpya imeonesha kundi la Wasichana wadogo akiwemo Mwanafunzi mwenye umri wa miaka 16 akigombezwa hadharani na kukamatwa kwa kosa la hilo na Polisi wa Korea Kaskazini.
Serikali inafuatilia vikali na kudhibiti mtiririko wa habari ndani ya mipaka yake, inakataza Raia kusikiliza miziki ya kigeni, filamu na tamthilia za kigeni ambapo wanaokiuka sheria hizo hukumbana na adhabu kali ikiwa ni pamoja na kuaibishwa hadharani, kufungwa gerezani na hata kunyongwa wakati mwingine.
Vyomvo vya habari vya Korea Kusini vinaendelea kupenya Korea Kaskazini kupitia Wanaharakati wa Kusini ambao hutuma USB zilizojaa Drama na Muziki kwa kutumia maputo.
Hii si mara ya kwanza kutekeleza adhabu hii kwani mwaka 2021 korea Kaskazini ilianzisha sheria mpya nia ikiwa ni kukabiliana na ushawishi wowote ule kutoka nje ya nchi hiyo huku adhabu kali ikitajwa kutolewa kwa yeyote atakayepatikana na filamu za nje ya nchi hiyo, mavazi au hata kutumia lugha ya mitaani.
Bwana Kim aliandika barua katika chombo cha habari kinachomilikiwa na serikali nchini humo, akitoa wito kuwa anataka kusitisha tabia “zisizofaa, ubinafsi na zisizopendelea ujamaa” miongoni mwa vijana.
Kim Anataka kusitisha maudhui kutoka nchi za kigeni, mitindo ya nywele na mavazi anayoelezea kama “sumu hatari”.