Korea Kusini imeanzisha uchunguzi kuhusu Mtandao wa Telegram kufuatia taarifa za uhalifu wa mtandaoni unaohusisha video za ngono hii ni ulingana na ripoti kutoka shirika la habari la Yonhap.
Uchunguzi huu utaangalia ikiwa Telegram ilihusika katika kusambaza maudhui ya picha na video za ngono zilizoundwa kwa kutumia teknolojia ya deepfake.
Mchunguzi mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Uchunguzi alithibitisha kuwepo kwa uchunguzi huo, huku afisa wa kitengo cha uchunguzi wa mtandao cha Polisi wa Taifa akiepuka kuthibitisha ripoti hiyo kwa simu. Hata hivyo, mamlaka ya Korea Kusini imetoa mwito kwa Telegram na majukwaa mengine ya mitandao ya kijamii kushirikiana katika kupambana na maudhui haya ya ngono.
Uchunguzi huu unatokana na ripoti kutoka vyombo vya habari vya ndani vinavyosema kuwa picha na video za ngono za wanawake wa Korea Kusini zimekuwa zikionekana mara kwa mara katika vyumba vya mazungumzo vya Telegram.
Taarifa hizi zimeongeza wasiwasi miongoni mwa mashirika ya haki za wanawake na wadhibiti wa mtandao.
Telegram haikupatikana mara moja kutoa maoni, lakini kampuni hiyo ilisema wiki iliyopita kwamba inachukua hatua madhubuti katika kudhibiti maudhui hatarishi kwenye jukwaa lake, ikiwemo picha za ngono zisizo halali.
Kampuni hiyo iliongeza kuwa, “Watendaji wetu wanatumia njia mchanganyiko za ufuatiliaji wa sehemu za umma za jukwaa, zana za AI za hali ya juu, na ripoti za watumiaji ili kuondoa vipande milioni vya maudhui hatarishi kila siku.”
Uchunguzi huu unakuja wakati ambapo Korea Kusini inakabiliwa na ongezeko la taarifa za uhalifu wa mtandaoni unaohusisha picha za ngono zinazozalishwa kwa teknolojia ya deepfake, ambayo ina athari kubwa kwa waathirika, hasa wanawake.
Serikali ya Korea Kusini ina matumaini kuwa uchunguzi huu utaweza kubaini iwapo Telegram imechukua hatua za kutosha kukabiliana na tatizo hili.