Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) amewataka wahitimu wa Chuo cha Taifa cha Utalii kuutangaza utalii kujipambanua kwa kuanza kutafuta masoko ya ajira hasa katika Sekta ya Utalii ilii kuutangaza utalii wa ndani.
Ameyasema hayo leo alipokuwa akihutubia kwenye Mahafali ya 19 ya Chuo cha Taifa cha Utalii yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa (JNICC) jijini Dar es Salaam.
“Watalii wanaendelea kuongezeka na hii ni nafasi yenu sasa wahitimu kwenda kuangalia masoko, kwa wale watakaopata ajira tunawaombea heri lakini kwa wengine watakaokosa ajira ya kujiajiri mwenyewe ni ajira nzuri na ajira mbadala” Mhe. Masanja amesisitiza.
Amewataka wahitimu hao kuacha kufikiria masoko ya utalii ya nje ya nchi na badala yake watangaze vivutio vilivyoko katika kila ngazi ya Wilaya na Kata nchini.
Aidha, amewaasa wahitimu hao kufikiria namna mbadala ya kujiajiri kwa kutumia ujuzi walioupata.