Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro linamshikilia Gervas Eliewaha Mgonja, (42), Mkazi
wa Moshi/Arusha, Mwenyekiti wa chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)
Mkoa wa Kilimanjaro kwa kosa la kutoa kauli za kuhamasisha Wananchi kuvamia
makazi ya Wasimamizi wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 wa Mkoa wa Kilimanjaro.
Akitoa taarifa hiyo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro Kamishna Msaidizi Mwandamizi Simon Maigwa amesema Mtuhumiwa huyo amekamatwa baada ya kuonekana kwa video mjongeo iliyosambaa
katika mitandao ya kijamii akiwa anawahamasiha Wananchi kufanya uhalifu huo
Novemba 27, 2024.
Maneno hayo ya kuhamasisha vurugu aliyatamka hadharani Novemba 24, 2024 na
baada ya kutamka waliyasambaza katika mitandao ya kijamii.
SACP Maigwa ameongeza kuwa mtuhumiwa huyo anachukuliwa maelezo ili hatua zingine za kisheria ziweze kufuata.
Sambamba na hilo Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro linatoa onyo kwa yeyote atakayethubutu kufanya
vitendo vyovyote vyenye viashiria vya uvunjifu wa amani kabla, wakati na baada
uchaguzi hatua stahiki za kisheria zitachukuliwa dhidi yake bila kumwonea muhali.