Waziri Mkuu wa Iraq Mohammed Shia al-Sudani alisema kuwa kundi la kigaidi la Islamic State (ISIS) halitoi tishio tena kwa Iraq na mazungumzo ya kumaliza muungano wa kimataifa unaoongozwa na Marekani kupambana na kundi la IS yanaendelea.
Al-Sudani ameyasema hayo katika mazungumzo yake na Meja Jenerali Kevin C. Leahy, kamanda wa muungano unaoongozwa na Marekani dhidi ya ISIS nchini Iraq mbele ya balozi wa Marekani nchini Iraq Alina L. Romanowski, imesema ofisi ya vyombo vya habari vya al-Sudani katika taarifa yake, shirika la habari la Xinhua liliripoti.
Mabaki ya magaidi wa ISIS wamegeuka na kuwa magenge ambayo yanawindwa na vikosi vya Iraq katika maeneo ya mbali ya nchi hiyo, ilisema taarifa hiyo.
Mkutano huo ulilenga “maendeleo ya mazungumzo ya kiufundi kati ya Iraq na muungano wa kimataifa unaoongozwa na Marekani kuhusu kukomesha ujumbe wa muungano huo nchini humo na kuhamisha ujumbe huo kwa uhusiano wa pande mbili kati ya Iraq na nchi wanachama wa muungano,” ilisema. Majadiliano hayo pia yalihusu ushirikiano unaoendelea katika mafunzo, kugawana utaalamu, na ushirikiano wa kijasusi na vikosi vya usalama vya Iraq, iliongeza.