Jina la kiungo wa kimataifa wa Burundi aliyewahi kuichezea Newcastle United ya England Gael Bigirimana (28) linazidi kuwa gumzo nchini na wengi wanalihusisha kwamba yuko mbioni kujiunga na Mabingwa wa Tanzania Yanga SC.
Gael azaliwa October 22 1993 Bujumbura Burundi Baba mrundi na mama mnyarwanda lakini ana uraia pacha kwa maana amewahi kuichezea timu ya Taifa ya England ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 (U-20) kabla ya 2015 kuamua kuanza kuitumikia Timu yake ya Taifa ya Burundi ambako ndio asili yake.
Bigirimana alianza kucheza professional 2011 akiwa anaichezea club ya Conventry City na mwaka mmoja baadae akasajiliwa na Newcastle Castle United ila hakuwa akipata nafasi ya kucheza sana na kujikuta akiishia kutolewa kwa mkopo katika vilabu vya Rangers, Conventry City kabla ya 2016 kurudi jumla Conventry na kukaa mwaka mmoja tu.
Maisha ya soka ya Bigirimana yakawa ya kudumu na vilabu kwa muda mfupi, kwani alijiunga na club ya Motherwell 2017 na 2019 akaondoka na kujiunga Hibernian aliyoishia kucheza game moja pekee, 2019-2020 akajiunga na Solhull Moors hakucheza mechi hata moja na kisha kujiunga na Grentoran 2020.
Sasa Gael Bigirimana ana husishwa kujiunga na Yanga japokuwa Viongozi wa Yanga hawajaweka wazi wala kudokeza chochote kuhusiana na taarifa hizo, ila zinazidi kuenea kwa kasi sana ukizingatia Yanga wametangaza kuwa watasajili wachezaji kati ya watano au nne wa kimataifa wakati huu wa dirisha la usajili.
Hadi sasa Yanga imetambulisha wachezaji wawili wa kigeni Lazaraus Kambole kutokea Zambia na Bernard Morrison wa Ghana huku Aziz Ki kutokea Burkinafaso utambulisho wake ukitarajia kufanyika muda wowote ndani ya wiki mbili zijazo. Hivyo kwa hesabu hizo na kwa mujibu wa mango wa Yanga watakuwa wamebakiza nafasi moja au mbili walizokusudia kusajili kama alivyonukuliwa afisa habari wao Haji Manara, tetesi zinavyoendelea huenda kweli Bigirimana akatua.
Kama ni kweli usajili wa Bigirimana kwenda Yanga una ukweli kuna maswali mengi ya kujiuliza yanayoleta utata kuhusiana na ubora wake, Bigirimana amekuwa akipata nafasi finyu ya kucheza katika vilabu kadhaa alivyopita barani Ulaya kiasi hata cha kukosa namba kabisa ya kucheza wakati mwingine, hiyo haiwezi kuwa ni kamari kwa Yanga kama ni kweli watafanya maamuzi ya kumsajili?
Swali jingine la kujiuliza ni kwamba kwa profile ya Bigirimana ya kusajiliwa au kuwahi kucheza katika timu ya Newcastle United ya Ligi Kuu ya England, anawezaje kukosa timu ya madaraja hata ya chini Ulaya na kuamua kujiunga na Yanga?
Sio dhambi wala kosa kwa Bigirimana kurudi Afrika kwenye asili yake kucheza soka la ushindani kama ilivyo kwa nyota wa zamani wa Cameroon na Arsenal Alex Song aliyeamua kujiunga na Arta Soler ya Djibouti lakini Song alijiunga na timu emri ukiwa umeenda, inawezekanaje Bigirimana akiwa na umri wa miaka 28 kuamua kurudi Afrika? umri ambao alipaswa kukipiga Ulaya au kwenda Ligi za wastaafu China na Marekani kuvuna pesa.
Bigirimana angeishi na kukulia Afrika tungeweza sema maisha Ulaya yamemshinda kama ilivyowahi kutokea kwa wachezaji kadhaa wa kitanzania waliowahi kwenda Ulaya na kushindwa maisha ya nje ya uwanja, GSM katoa ofa nono ya kumshawishi Bigirimana arudi Afrika? hayo yote ni maswali juu ya uwezo wake ila kwa uchumi wa vilabu na Ligi yetu sidhani kama ni ofa nono ndio inamleya Bigirimana Tanzania ila anaweza kuwa kiwango kimeshuka au ameandamwa na majeruhi ya mara kwa mara, tusubiri wananchi wamalizie utambulisho wa wachezaji wao kujua ukweli wa hadithi ya Bigirimana.