Waziri wa Maji Jumaa Aweso _amewataka wahandisi wa maji kutimiza majukumu yao ya kukamilisha miradi ya maji katika maeneo mbalimbali nchini kwa wakati ili wananchi wa maeneo husika kunufaika na miradi hiyo kwa kuondokana na changamoto ya maji.
Waziri wa Aweso ameyasema hayo siku ya Jumatatu Desemba 23, 2024 katika eneo la Komungu, kitongoji cha Mpande cha kijiji cha Kwamsisi kilichopo katika kata ya Kwamsisi, wilayani Handeni mkoani Tanga kutokana na agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan la kumtaka Aweso ahakikishe changamoto ya upatikanaji wa maji safi katika eneo hilo inatatuliwa.
“Mimi ninafika hapa mitaro imekwishachimbwa, maji yapo karibu kufika kwa wananchi takribani kilomita moja tu, Ninataka niwaambie sina lugha nyingine, wahandisi wa maji msizoee shida za wananchi na kuona kitu cha kawaida”, ameeleza Waziri Aweso.
Ametoa maelekezo kwa Meneja wa Wakala ya Usambazaji Maji na Usafi na Mazingira Vijijini (RUWASA) wilaya ya Handeni, Hosea Mwingizi, ahakikishe maji yaliyopatikana kutokana na mradi wa World Vision yanawafikia wananchi pamoja na taasisi za eneo hilo kama msikiti huku akitoa siku saba kukamilika kwa jambo hilo.
Aidha amewaelekeza wahandisi wa maji mkoa wa Tanga na meneja wa maji wilaya ya Handeni kuwezesha mradi mwingine uliopo katika kata ya Kwamsisi kufanya kazi kwa ufanisi kwa kupatiwa huduma ya umeme kwani kwa sasa mradi huo unategemea nishati ya jua.
Amesema Rais Samia alipompa jukumu la kusimamia sekta ya maji, alimtaka kuhakikisha kuwa wananchi hawateseki kwa shida ya maji na katika hilo amemshukuru Rais kwa kuwezesha utatuaji wa changamoto ya maji katika maeneo mbalimbali nchini.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Tanga Balozi Dkt. Batilda Burian amesema kutokana na Rais Samia kuguswa na changamoto ya maji, nusu ya Shilingi trilioni 1.8 iliyopatiwa mkoa huo imeelekezwa kutatua changamoto hiyo.
Kutokana na dhamira ya Rais, ameahidi mgogoro wa umiliki wa ardhi ulioelezwa kuwepo kati ya mwekezaji na wananchi, na kutajwa kuwa moja ya changamoto zinazokwamisha kuendelezwa kwa mradi wa maji katika eneo hilo, kwamba utatatuliwa kwa njia ya ushirikishwaji wa pamoja na wa moja kwa moja wa wananchi kwani mwekezaji yupo tayari kukaa na wananchi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wananchi wa kijiji cha Kwamsisi wamemshukuru Rais Samia kwa kuonesha kuguswa na changamoto zinazowakabili kwa kutoa maagizo ya kuchukuliwa hatua za haraka za kutatua adha hiyo. Aidha wametaka maagizo yaliyotolewa na Waziri Aweso katika ziara hiyo yafanyiwe kazi ili wapate maji.
Hata hivyo Fatuma Ali, amesema kuwa baada ya mradi wa World Vision kukamilika ulikabidhiwa kwa kijiji, na ikasemekana kuwa pesa tayari zimetoka lakini anashangaa hali ya mambo kuonekana kusuasua.
Naye Nandima Ramadhani, amesema changamoto ya maji si ya Kwamsisi pekee bali kata nzima, kwani miradi kadhaa katika kata hiyo haiendelezwi.
Aidha amewataka viongozi wafuate mnyororo pale ambapo kunatakiwa kushirikishwa wananchi au viongozi basi washirikishwe.