Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imetangaza kuanza kutumika rasmi kwa nauli za mabasi ya masafa marefu na mijini (daladala) ambazo zimepanda, kuanzia leo ljumaa, December 08, 2023.
Taarifa hii inarejea Amri ya Bodi ya LATRA iliyotangazwa kwenye Gazeti la Serikali (Taarifa ya Kawaida Na. 6935), Toleo Na. 47 la tarehe 24 Novemba, 2023 (rejea Kiambatisho Na. 1), taarifa hii pia inazingatia kuwa hadi kumalizika siku 14 tangu Amri ya Bodi ya LATRA itangazwe, hakukuwa na pingamizi la kisheria didi ya amri hiyo.
Itakumbukwa November 27,2023 LATRA ilitangaza ongezeko la nauli kwa mabasi ya mjini ya masafa mafupi na mabasi ya safari za masafa marefu baada ya kupitia maoni ya Wadau wa usafiri nchini ambapo nauli za safari zisizozidi KM 10 nauli yake itakuwa Tsh. 600 kutoka Tsh. 500.
“Kwa safari za KM 11 hadi 15 ambayo nauli yake ilikuwa Tsh. 550 sasa itakuwa Tsh. 700 na kwa KM 15 hadi 20 ambapo nauli ilikuwa Tsh. 600 sasa itakuwa 800 huku kwa safari za KM 21 hadi 25 nauli ikitoka Tsh. 700 hadi Tsh. 900”
“Safari ya KM 26 hadi KM 30 nauli ni Tsh. 1100, safari ya KM 31 hadi 35 ni Tsh. 1300 na KM 36 hadi 40 nauli ni Tsh. 1400, nauli za Wanafunzi zitaendelea kusalia 200 kwa safari za masafa mafupi”