Wabunge wameiomba Serikali kuupitia upya mkataba wa miradi ya chuma na makaa ya mawe ya Liganga na Mchuchuma ulioingiwa kati yake na Kampuni ya Schwang Holder ya China kutokana na kuwa na harufu ya ufisadi wakati wa uingiwaji wake.
Wabunge hao akiwemo Stanslaus Nyongo na Christopher Ole Sendeka wameiomba serikali kupitia upya Utekelezaji wa mradi huo kati yake na mwekezaji ili kuondoa dosari inayoashiria ufisadi ndani ya mkataba.
Hoja hiyo imeibuka wakati Mbunge wa Kawe Askofu Josephat Gwajima akitoa mchango wake ambapo Wabunge hao walisimama na kuupinga ushauri wa Askofu Gwajima aliyetaka mkataba huo kutositishwa kwasababu utaipatia Serikali fedha nyingi.
Kwa upande wake Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dr. Ashatu Kijaji aliingilia kati na kubainisha kuwa Serikali inawafuatilia Watendaji wote waliohusika na uingiaji wa mkataba huo.
Akifafanua Dr. Kijaji ameongeza kuwa walimwita Mwekezaji huyo zaidi ya mara tano ili kuzungumza nae juu ya dosari za mkataba huo usioendana na sheria za nchi lakini hakufika na ili kwenda na kasi ya Serikali ya awamu ya sita itaachukua uamuzi wenye maslahi kwa taifa ambao hautaliumiza Taifa wala Mwekezaji.