Top Stories

Wafanyabiashara ya Utalii Rwanda na Tanzania kuunganishwa

on

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Rwanda imekubaliana kuwaunganisha wafanyabiashara wa Sekta ya Utalii wa nchi hizo ili kukuza utalii.

Hayo yamesemwa leo na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja (Mb) katika Maadhimisho ya Wiki ya Utalii ya Rwanda yanayoendelea nchini humo.

“Kikubwa tumeweza kukutana na Rais wa wafanyabiashara za kitalii wa hapa nchini Rwanda na tumeomba wafanyabiashara wa huku kushirikiana na wa kwetu kukuza Sekta ya Utalii” Masanja.

Aidha, Masanja amewataka Watanzania kuwa wazalendo kwa kutangaza vivutio vya utalii vilivyoko nchini mwao.

Nawaomba Watanzania kwa umoja wetu tuendelee kuwa wazalendo, tuipende nchi yetu na tuendelee kuitangaza nchi yetu kama ambavyo wenzetu wa Rwanda wanavyofanya” Masanja amesisitiza.

Naye, Naibu Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Maendeleo ya Rwanda, Zephanie Niyonkuru amesema kuwa Maadhimisho ya Wiki ya Utalii ya Rwanda yamelenga katika kuibua ubunifu katika Sekta ya Utalii nchini humo na kutoa tuzo kwa mshindi.

Ameongeza kuwa pia maonesho hayo yanatoa fursa kwa wafanyabiashara wa ndani na wa Kimataifa kuuza bidhaa na huduma zao kwa wadau wengi kutoka Bara la Afrika.

Kwa upande wake Afisa Masoko Mkuu kutoka Bodi ya Utalii Tanzania, Bernard Mtatiro amesema kupitia Wiki ya Utalii ya Rwanda Tanzania itapata fursa ya kutangaza mazao mapya ya utalii kwa nchi zote za Jumuiya ya Afrika Mashariki.

“Tumejipanga kutangaza mazao mapya ya utalii kwa mfano Utalii wa Mchezo wa gofu, reli ya mwendokasi (SGR), Bwawa la umeme la Mwalimu Nyerere na Hifadhi ya Taifa ya Nyerere” Mtatiro.

Maadhimisho hayo yenye kaulimbiu ya “Kujenga Upya Utalii kwa Ukuaji Endelevu”yamehudhuriwa na washiriki kutoka nchi za Tanzania, Ghana, Botswana Kenya, Nigeria, Kongo, Afika Kusini, Somalia, Zimbwabwe pamoja na wadau wa utalii kutoka Dubai.

Soma na hizi

Tupia Comments