Serikali imetangaza rasmi kuanza kwa ujenzi wa Kampasi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mapema mwezi December mwaka huu katika eneo la Gongo kata ya Jamhuri Mkoani Lindi, ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia kuhakikisha Mikoa yote ambayo haina Vyuo Vikuu inajengewa kampasi za Vyuo Vikuu.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda amesema akiwa Mkoani Lindi amesema “Leo nimekuja kutangaza rasmi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kimekamilisha taratibu za kikanuni na kisheria za kuanzisha kampasi, kutakuwa na kampasi ya Chuo hicho hapa Lindi na kitaanza na Wanafunzi 360”
Ametaja Mikoa mingine itakayojengewa kampasi za Vyuo Vikuu kuwa ni Kagera, Mwanza, Shinyanga, Singida, Manyara, Tanga, Simiyu, Kigoma, Ruvuma, Rukwa Katavi, na Zanzibar (Institute of Marine Scince) na kwamba kampasi hizo zinajengwa na Mradi wa Kuendeleza Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET).
Waziri Mkenda amevitaka Vyuo Vikuu vitakavyojenga kampasi hizo kuzielekeza kwenye kutoa mafunzo ya amali lakini pia kufanya tafiti na amekipongeza Chuo Kikuu hicho kwa kukamilisha taratibu hizo lakini pia Mkoa wa Lindi kwa kutoa ushirikiano wa kuhakikisha ujenzi wa Chuo unaanza.