Mfanyabiashara Mbutusyo Mwakihaba (40) amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na kosa la kusambaza taarifa za uongo kwamba amemuona Kachero karibu na Hospitali aliyolazwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu.
Mshtakiwa huyo alisomewa kosa lake mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Victoria Nongwa na Wakili wa Serikali, Janeth Magoho.
Wakili huyo wa Serikali alidai kuwa September 11, 2017 huko Dar es Salaam kupitia mfumo wa kompyuta alisambaza taarifa hiyo kwenye mtandao wa kijamii wa WhatsApp.
Mshtakiwa huyo anadaiwa kusema “Huyo ni Kachero wa Usalama wa Taifa anatambulika kwa jina la Jose ameonekana Nairobi karibu na Hospitali aliyolazwa Mbunge wa Singida Mashariki, Mh Tundu Lissu mwacheni mwenzenu.”
Wakili huyo wa Serikali, Magoho alidai kuwa mshtakiwa aliyatoa maneno hayo kwa nia ya kupotosha umma ambapo baada ya kusomewa shtaka hilo, mshtakiwa alikana na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi bado haujakamilika.
Hakimu Nongwa alimtaka mshtakiwa huyo kuwa na wadhamini wawili wanaoaminika ambao kila mmoja anatakiwa kusaini bondi ya Tsh Milioni 5 ambapo kesi imeahirishwa hadi October 12, 2017 kwa ajili ya kutajwa na mshtakiwa ameshindwa kukamilisha masharti hayo ya dhamana na kupelekwa rumande.
Viongozi wa juu CHADEMA wazungumzia hali Tundu Lissu kwa sasa