Mfanyabiashara wa Kariakoo, Casto Ngogo mwenye umri wa miaka 35 amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na kosa la kukutwa na suruali 5,000 za Jeshi la Wananchi (JWTZ), t-shirt na vitu.
Mshtakiwa amesomewa mashtaka yake na Wakili wa Serikali, Wankyo Simon mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba ambapo amedai kuwa Ngogo ambaye ni mkazi wa Tabata Segerea, June 15, 2017 alikutwa na vifaa vya JWTZ katika maeneo ya Bandari kavu ya Galco Inland Container (ICD) iliyopo Sokota Chang’ombe.
Wakili Simon amedai siku hiyo, mshtakiwa alikutwa na suruali 5,000 za JWTZ zenye thamani ya Tsh. Milioni 50 ambazo zimepatikana kwa njia isiyo halali.
Ngogo anadaiwa pia June 15, 2017 katika eneo hilo alikutwa na Maofisa wa Jeshi la Polisi akiwa na t-shirt 50 za JWTZ zenye thamani ya Tsh. 500,000.
Pia inadaiwa kuwa June 17, 2017 mshtakiwa akiwa katika eneo African Inland Container Deport alikutwa na Polisi akiwa na jozi 20 za viatu vya JWTZ bila ya kuwa na uhalali.
Mshtakiwa hakuruhusiwa kuongea chochote kwa sababu makosa yanayomkabili, Mahakama hiyo haina mamlaka kuyasikiliza hadi Mahakama Kuu.
Aidha, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) amewasilisha hati ya kumzuia mshtakiwa asipiwe dhamana chini ya kifungu cha 36 (2) cha sheria ya uhujumu uchumi ambapo kesi imeahirishwa hadi August 29, 2017 kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wa kesi bado haujakamilika.
ULIPITWA? Wafuasi wa CUF waliodhibitiwa Mahakamani…tazama kwenye video hii hapa chini!!!