Dunia imeadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kukumbuka Kutokomezwa Biashara ya Utumwa ambapo walimwengu wameangazia mateso na madhila waliyokumbana nayo watu wenye asili ya Afrika mikononi mwa wafanyabiashara ya utumwa.
Msingi wa siku hii ni usiku wa tarehe 22 kuamkia tarehe 23 mwezi Agosti mwaka 1791 huko Saint Domingue, leo hii ikijulikana kama Haiti ambako kulishuhudiwa mwanzo wa vuguvugu ambalo lilikuwa na dhima muhimu katika kutokomezwa biashara ya utumwa ya kuvuka bahari ya Atlantiki.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO, ambalo ndilo lilipitisha siku hii kupitia mkutano wake mkuu wa 29 tarehe 29 Julai mwaka 1998, linasema kitendo hicho ndio msingi wa maadhimisho ambayo hufanyika tarehe 23 mwezi Agosti kila mwaka.
Kwa mara ya kwanza, maadhimisho yalifanyika katika nchi kadhaa ikiwemo Haiti tarehe 23 Agosti 1998, na kisiwa cha Gorée nchini Senegal tarehe 23 Agosti mwaka 1999.
Siku hii inalenga kuonesha janga la biashara ya utumwa katika kumbukumbu za watu.
Kwa mujibu wa mradi wa tamaduni mbali mbali unaoitwa “Njia za watumwa,” siku hii inapaswa kuwa fursa ya kuchunguza sababu za kihistoria, mbinu na madhara ya janga la utumwa barani Afrika, Ulaya, Amerika na Karibea.
Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO, Audrey Azoulay akizungumzia kuhusu siku hii amesema, “ni wakati wa kutokomeza kabisa utumikishaji wa binadamu na kutambua utu sawa na usio na masharti kwa kila mtu. Leo hii hebu na tukumbuke waathirika, wapiganaji wa zamani ili waweze kuwa hamasa kwa vizazi vijavyo katika kujenga jamii zenye usawa.”