Maelfu ya Waislamu wa jamii ya Rohingya wameandamana katika kambi za wakimbizi kusini mwa Bangladesh katika maadhimisho ya sita ya mauaji ya halaiki dhidi yao.
Wakimbizi hao wanataka haki itendeke kufuatia kamatakamata na mauaji yaliyofanywa na jeshi la Myanmar dhidi yao miaka sita iliyopita.
Shirika la amani na haki za binaadamu la Arakan Rohingya ndilo lililoandaa maandamano hayo katika kambi 34 za wakimbizi, ambazo ni makao ya zaidi ya Warohingya milioni moja waliokimbia mateso nchini kwao, Myanmar.
Umoja wa Mataifa unasema mwaka 2022 ulikuwa mmoja wa miaka mbaya zaidi kwa Warohingya baharini baada ya karibu wakimbizi 400 kuangamia walipokuwa wakifanya safari za hiana za boti kutoka Myanmar na Bangladesh kuvuka Bahari ya Andaman na Ghuba ya Bengal.
Jeshi la Myanmar lilianza kuwaua wanaume wa Rohingya, kuwabaka wanawake na kuchoma vijiji vyao siku hiyo, zaidi ya 750,000 kati yao walikimbilia nchi jirani ya Bangladesh ambako walikuwa wamehifadhiwa katika wilaya ya kusini ya Cox’s Bazar – ambayo sasa ni kambi kubwa zaidi ya wakimbizi duniani.