Siku ya Watoto Duniani ilianzishwa kwa mara ya kwanza kunako mwaka wa 1954 kama Siku ya Watoto Wote na huadhimishwa na Jumuiya ya Kimataifa tarehe 20 Novemba ya kila mwaka ili kukuza umoja, mshikamano na mafungamano ya kimataifa, ufahamu miongoni mwa watoto duniani kote, na kuboresha ustawi, maendeleo na mafao ya watoto wote.
Tarehe 20 Novemba 1959 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha Tamko la Haki za Mtoto na Mwaka 1989 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha Mkataba wa Haki za Mtoto.
Tangu 1990, Siku ya Watoto Duniani pia inaadhimisha kumbukumbu ya tarehe ambayo Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha Azimio na Mkataba wa haki za watoto.
Hii ni siku muhimu sana kwa maisha ya watoto kijamii na Kimataifa.
Hii ni siku ya kusimama kidete kutetea, kukuza na kudumisha haki msingi za watoto kwa kutafsiri haki hizi kwa vitendo vinavyopania kuboresha ulimwengu wa watoto.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Watoto (UNICEF) limetoa ripoti inayoelezea hali itakavyokuwa kwa watoto katika mwaka 2050 kwa kuzingatia hatari na maendeleo ambayo wanaweza kukumbana nayo.
UNICEF inasema kutokana na hatua za maendeleo zilizopigwa katika sekta za matibabu na teknolojia, idadi ya vifo vya watoto itaendelea kupungua.
Kufikia mwaka 2050, kiwango cha kuishi kwa watoto wachanga kinatarajiwa kufikia 98% na takriban 99.5% ya watoto wanaonusurika vifo wanapozaliwa, wanakadiriwa kuishi kwa zaidi ya umri wa miaka mitano.