Maafisa Habari kutoka Wizara, Taasisi, Halmashauri na Wakala mbalimbali za Serikali Februari 19, 2024 walitembelea Mgodi wa Kiwira, Wilaya ya Tukuyu Mkoani Mbeya kama sehemu ya mafunzo ya kutoa elimu kwa umma.
Ziara hiyo ilikuwa sehemu ya juhudi za kuhamasisha matumizi ya nishati safi, ikiwa ni mkakati wa Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuongeza matumizi ya nishati safi kwa maendeleo endelevu.
Akizungumza katika ziara hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) Dkt. Ayoub Rioba Chacha alisema kuwa Serikali inatoa msukumo mkubwa kwa wananchi na viwanda kutumia nishati safi, huku akiutaja mgodi wa Kiwira kama mfano wa mafanikio katika uendelezaji wa nishati safi.
“Mhe Rais anazungumzia matumizi ya nishati safi, na tayari kama nchi tumefufua kiwanda chetu cha Kiwira, ambacho sasa kinasimamiwa na watanzania wenzetu, lengo ni kuhakikisha soko la ndani linaimarika na wanakuwa na mkaa wa kutosha,” alisema Dkt. Rioba.
Vilevile, alisisitiza kuwa mkaa unaozalishwa na Kiwira ni bora zaidi ukilinganisha na mkaa mwingine, na kuonyesha kuwa ni hatua nzuri katika kuboresha mazingira na kudhibiti matumizi ya kuni.
Kwa upande wake, Mhandisi Peter Maha
Mratibu wa Mradi wa Makaa ya Mawe Kiwira -Kabulo amesema Kuwa Mgodi huo ulianza rasmi mwaka 1980 kwa ajili ya uchimbaji wa makaa ya mawe kwa uzalishaji wa umeme na matumizi ya viwandani.
Alisema awali, Serikali ilitoa fedha kwa ajili ya ulinzi wa miundombinu, lakini hivi sasa, kiwanda hicho kimefufuka na kimekuwa sehemu ya dhamira ya Serikali ya kuendeleza matumizi ya nishati safi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, washiriki wa ziara hiyo walieleza kuridhishwa na hatua zinazochukuliwa katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi, hususan kwa kutumia mkaa wa Kiwira kwa ajili ya kupikia kwa kutumia makaa ya mawe hivyo, kusaidia kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa katika maandalizi ya chakula.
Walisisitiza kuwa ni muhimu kwa jamii kuendelea kujifunza na kutekeleza mbinu bora za utunzaji wa mazingira ili kuendeleza ustawi wa taifa.
Wakiwa katika mgodi huo, maafisa hao walijionea mabadiliko makubwa yaliyofanywa katika kiwanda cha Kiwira, ambacho kilikumbwa na changamoto nyingi tangu kuanzishwa kwake mwaka 1980.