Serikali ya Urusi imewaambia Maafisa waliohusika katika maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2024 wa nchini humo kuacha kutumia simu za iPhone ambazo ni za kampuni ya Marekani ya Apple kwa sababu ya wasiwasi kwamba vifaa hivyo vinaweza kudukuliwa na Mashirika ya kijasusi ya Magharibi.
Katika semina iliyoandaliwa na Serikali ya Urusi kwa Maafisa wanaohusika na siasa za ndani ya Nchi hiyo, Sergei Kiriyenko ambae ni Naibu Mkuu wa kwanza wa utawala wa Rais, aliwataka Maafisa hao kubadilisha simu zao ifikapo April 1, 2023.
Kwa upande mwingine, Msemaji wa Serikali ya Urusi Dmitry Peskov aliwaambia Waandishi wa Habari kuwa simu janja (smart phones) hazipaswi kutumika katika masuala rasmi ya kitaifa kwani zinahofiwa kudukuliwa kudukuliwa kutokana na mifumo yake bila kujali ni mfumo gani wa uendeshaji iwe ni android au iOS.
Rais Vladimir Putin wa Urusi alisema kuwa yeye binafsi hatumii smartphone na vilevile Peskov amenukuliwa akisema Rais huyo hutumia mtandao wa Internet mara chache japo rekodi kadhaa za baada ya Urusi kuanza vita yake nchini Ukraine mwaka jana, Majasusi wa Marekani na Uingereza walidai kufichua na kuweka hadharani mpango mzima wa Putin kutaka kuivamia Ukraine lakini haijulikani ni jinsi gani Majasusi hao walipata taarifa hizo.