Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, jijini Dar es Salaam, imeitaka Jamhuri kutimiza wajibu wake wa kuleta mashahidi katika kesi ya ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu.
Amri hiyo imetolewa leo Alhamisi, Januari 20, 2022, na Jaji Joachim Tiganga anayesikiliza kesi hiyo, baada ya Jamhuri kushindwa kuleta shahidi mwingine.
Ni baada ya shahidi wao wa 10, Mchunguzi wa Kitengo cha Uchunguzi wa Kisayansi cha Jeshi la Polisi, Inspekta Innocent Ndowo, kumaliza mapema kutoa ushahidi wake.
Shahidi huyo aliyeanza kutoa ushahidi wake Jumatatu ya tarehe 17 Januari 2022, amemaliza kutoa ushahidi wake leo Alhamisi Saa 5 kasoro asubuhi, ambapo kwa mujibu wa taratibu za mahakama hiyo, kesi husikilizwa hadi saa 11.00 jioni.
“Kwa sababu hiyo niielekeze upande wa mashtaka kutimiza wajibu huu, kesho walete shahidi kesi iweze kuendelea kwa sababu wanao muda wa kutosha,” amesema Jaji Tiganga
“Kwa maelekezo hayo, upande wa mashtaka walete shahidi kesho, ili kesi iweze kuendelea, pale kutakapokuwa na sababu kuonekana shahidi ana dharura, mfanye utaratibu mapema wa kuleta shahidi mwingine,” amesisitiza
Jaji Tiganga amesema kukosekana kwa shahidi kunachelewesha ushahidi kumalizika.
“Kwa amri nimetoa siku mbili nilielekeza upande wa mashtaka waite shahidi mwingine sambamba na shahidi aliyekuwa anatoa ushahidi.
Jana ilikuwa ngumu sababu sehemu kubwa ya ushahidi wake alikuwa hajautoa, lakini kwa namna ambavyo ushahidi wake ulivyokuwa jana na uliobaki, ilikuwa wazi usingechukua siku nzima,” amesema Jaji Tiganga na kuongeza:
“Kwa sababu hiyo ilitegemewa upande wa mashtaka kutekeleza amri kwa kuanza na shahidi mwingine, lakini wamekuja na maelezo kwamba shahidi waliyemtegemea hakuweza kufika jana na wakasema walifanya maamuzi kuita shahidi mwingine wa nje ya Dar es Salaam na shahidi huyo atafika leo.”
Jaji Tiganga alitoa amri hiyo, baada ya Kiongozi wa Jopo la Mawakili wa utetezi, Peter Kibatala, kupinga ombi la Wakili wa Serikali Mwandamizi, Robert Kidando, la kesi hiyo kuahirishwa kutokana na shahidi waliyepanga kumleta kupata dharura.