Waziri mkuu kasim majaliwa ameliagiza jeshi la uhamiaji nchini kutembelea na kufanya ukaguzi kwenye vituo vya uandikishaji na uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura ili kuwabaini watu wasio watanzania wanaotaka kujipenyeza kuandishwa kwenye daftari hilo.
Waziri Majaliwa amesema hayo katika uzinduzi wa kuboresha daftari la kudumu la wapiga kura uliofanyika katika uwanjwa wa Kawawa manispaa ya Kigoma Ujiji.
Amesema mwananchi ndiye mtu wa kwanza kutambua nani ni mtanzania na nani si mtanzania katika maeneo wanaoishi hivyo kuwe na ushirikiano baina yao ili kutambua wasio na sifa ya utanzania kuwa hawajiandikishi katika daftari hilo na kufanya zoezi hilo kufanyika kwa ufanisi mkubwa.
“Watanzania lazima tuwe wazalendo, upigaji kura ni kwa sisi watanzania, tunachagua viongozi watakaoliongoza taifa la Tanzania, tunachagua viongozi ambao watakuja kuwa viongozi wa mitaa yetu na vitongoji vyeti, kwanini kuruhusu mtu wa nje aje atupigie kura? Atatuamlia ambavyo sisi hatutaki, kwahio tusiruhuri mtu yoyote kutoka nje ajiandikishe katika daftari la mpiga kura”
Amesema kila mtanzania asimamie zoezi hilo kwa uadilifu kutoa taarifa sahihi za raia anayetaka kujiandikisha ambaye si mtanzania kwani zoezi hilo ni la watanzania pekee na si vinginevyo.
Vile vile amewataka viongozi wa vyama vya siasa kuweka mawakala watakaosimamia zoezi hilo kutoka katika kijiji husika kwakuwa ndiye anayewafahamu wananchi wa eneo hilo na hivyo kuwa rahisi kutambua ambao hawana sifa za kuandikisha kama raia wa Tanzania.
“Naomba mawakala wote muwe wazalendo na makini kuangalia kila anayekuja kuboresha taarifa zake na kufuatilia namna anavyohojiwa kwakuwa maelezo yake yanaweza kutusaidia kutambua aliye raia na asiye raia” Alisisitiza Majaliwa.
Hivyo hivyo amewataka watendaji na wote watakaohusika katika zoezi la uandikishaji kutumia lugha nzuri, kutoa maelekezo mazuri ,na kutekeleza wajibu huo kwa kuzingatia sheria na taratibu zinazotolewa na tume na kwamba wahakikishe zoezi hilo linakamilika pa bila kuwa na dosari yoyote.
Akizungumza Ummy Ndariananga naibu waziri ofisi ya waziri mkuu sera, bunge na uratibu amesema mchakato wa uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura umeshirikisha wadau mbalimbali wa uchaguzi ikiwa ni utekelezaji wa falsafa ya 4R ya mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan.
amesema lengo la kufanya hivyo ni kuhakikisha mchakato unakuwa shirikishi kwa watanzania wote bila kujali itikadi za vyama vya siasa au dini.
Awali akitoa taarifa kwa Waziri Mkuu, Mwenyekiti wa Tume huru ya Taifa ya uchaguzi nchini (INEC), Jacob Mwambegele alisema kuwa Katika uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mwaka huu 2024 kutakuwa na jumla ya vituo 40,126, ambapo kati ya vituo hivyo, 39,709 ni vya Tanzania Bara na vituo 417 ni vya Zanzibar.
Jaji Mwambegele alisema kuwa hilo ni ongezeko la vituo 2,312 ikilinganishwa na vituo 37,814 vilivyotumika kuandikisha wapiga kura mwaka 2019/2020 huku kukiwa na ongezeko la wapiga kura wapya milioni 5.5,wapiga kura milioni 4.3 wataboresha taarifa zao na wapiga kura 594,494 wataondolewa kwenye Daftari kwa kukosa sifa za kuendelea kuwepo kwenye Daftari hivyo baada ya uboreshaji inatarajiwa kuwa Daftari litakuwa na jumla ya wapiga milioni 34.7.