Polisi nchini Nigeria wanajiandaa kwa maandamano zaidi hivi leo ambapo hapo jana walilazimika kutumia risasi na mabomu ya kutoa machozi kukabiliana na waandamanaji waliojitokeza barabarani kupinga hali mbaya ya uchumi wa taifa hilo.
Katika maandamano hayo, watu kadhaa walikamatwa na wengine mamia kujeruhiwa huku watatu wakiripotiwa kupoteza maisha.
Maandamano haya ya nchi nzima yaliyopewa hashtag ya “maliza utawala mbovu Nigeria” yalipata uungwaji mkono mkubwa kutoka kwenye mitandao ya kijamii ambapo maelfu ya raia waliitikia wito na kujitokeza nchi nzima.
Maandamano ya hapo jana yamefanyika licha ya mwito wa rais Bola Tinubu, kutaka mazungumzo na vijana ili kupata ufumbuzi wa changamoto za kiuchumi zinazoikabili nchik hiyo, maandamano haya yakichochewa na kilichofanywa na vijana wa Gen Z nchini Kenya.
Raia wa Nigeria, wanakabiliwa na hali mbaya ya kupanda kwa gharama ya maisha, huku mfumuko wa bei za vyakula ukifikia asilimia 40 na bei ya mafuta ikipanda mara tatu zaidi ukilinganisha na mwaka uliopita, huku wengi pia wakihofia hali ya usalama.