Mjadala wa kutaka jina la Nchi ya Nigeria libadilishwe umeendelea kuwa gumzo nchini humo wakati huu ambapo Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wanaendelea kukusanya mapendekezo ya kubadili Katiba, hii ni baada ya Raia mmoja aitwaye Adeleye Jokotoye kupendekeza jina la Nchi hiyo kuwa United African Republic (Jamhuri ya Muungano Afrika).
Jokotoye amesema sababu ya kuomba jina lirudiwe kupitishwa upya ni kwakuwa jina hilo ni la Kikoloni ambalo wakati linapitishwa yeye hakuwepo halikupendekezwa kwa matakwa ya Wanaigeria ila llilipendekezwa karne ya 19 na Mwandishi wa Habari wa Uingereza, Flora Shaw, ambaye baadaye aliolewa na Msimamizi wa Kikoloni, Frederick Lugard.
Bashir Ahmad ambaye ni Msaidizi wa Rais wa Nigeria amesema anashangazwa kuona Watu wameanza kumtupia lawama Rais Muhammadu Buhari wa Nchi hiyo kuhusu mapendekezo hayo wakati aliyependekeza ni Raia na wala sio Rais wala sio Serikali.