Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema mabadiliko ya sera za Rais wa Marekani Donald Trump yanaifanya Tanzania iendelee kujiimarisha na kuwa na uwezo wa ndani na kuondoa utegemezi ili isitokee athiri na kuwataka Watanzania kutumia rasilimali za ndani ili kujenga uchumi.
Waziri mkuu Majaliwa kauli hiyo bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Mbozi, George Mwenisongole ambaye alitaka kufahamu kuhusu mipango ya serikali kulingana na mabadiliko ya sera za nje ya nchi ambazo zinatajwa kuathiri sera za elimu, afya na uchumi za Tanzania.
“Ni kweli kwamba serikali yetu inaheshimu sera za mambo ya nje na tunatekeleza mikataba kwa mujibu wa sera hizo kama ambavyo tumekubaliana na nchi hizo kwenye maeneo mbalimbali, tumeanza kuona nchi zenye uwezo mkubwa ikiwemo Marekani kubadilisha sera zao, na mabadiliko hayo yanaathiri baadhi ya nchi lakini pia hata nchi yetu inaweza kupata athari”. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
“Muhimu kwetu ni kuhakikisha kwamba tunajiimarisha kwa kuwa na uwezo wa ndani ili kuhakikisha kwamba hatuendelei kuwa wategemezi, ni lazima tujiimarishe kwenye mipango yetu, bajeti zetu ziweze kumudu kutekeleza maeneo yote ikiwamo maeneo hayo ya afya pamoja na elimu” PM Majaliwa.