Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) amezihimiza balozi za Tanzania nchi mbalimbali kushirikiana na Wizara yake katika kutangaza vivutio vya utalii.
Ameyasema hayo leo kwenye kikao na Balozi wa Tanzania nchini Rwanda, Mhe. Meja Jenerali Richard Makanzo alipotembelea ubalozi huo.
Mhe. Masanja amesema kupitia balozi za Tanzania, utalii unaweza kukua kwa kiasi kikubwa.
“Mkishiriki katika matukio mbalimbali hapa nchini Rwanda na kutumia vipeperushi na majarida kuutangaza utalii wetu, idadi ya watalii itaongezeka” Masanja.
Aidha, Mhe. Masanja ameutaka ubalozi huo kujenga mahusiano mazuri na wafanyabiashara wa sekta ya utalii na wawekezaji nchini Rwanda ili wavutiwe kuwekeza nchini Tanzania hasa katika maeneo ya fukwe na hifadhi ili kuiendeleza sekta hiyo.
Naye Balozi wa Tanzania nchini Rwanda, Mhe. Meja Jenerali Richard Makanzo amesema ofisi yake iko tayari kutoa ushirikiano kuhakikisha utalii wa Tanzania unakua.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Idara ya Utalii, Philip Chitaunga ameahidi kutoa ushirikiano kwa balozi za Tanzania za nchi mbalimbali ili kukuza utalii.
“Nitashirikiana na balozi kwa kuhakikisha vipeperushi, majarida, video na taarifa zozote zinazoongelea utalii wa Tanzania zinapatikana kwa urahisi” Chitaunga amesisitiza.
Amesema kuwa ni muhimu ubalozi wa Tanzania nchini Rwanda kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii ili kuwezesha watalii wanaokuja Rwanda waweze kutembelea Tanzania bila vikwazo.
Mary Masanja yupo nchini Rwanda kwa ajili ya kushiriki Kongamano la Uongozi wa Utalii Afrika na Tuzo za Wiki ya Kusafiri litakalofanyika kesho kwenye hoteli ya Kigali Serena.