Shirika la Reli Tanzania – TRC linautaarifu umma kuwa mabehewa 264 ya mizigo yatakayotumika katika reli ya kiwango cha kimataifa – SGR yamewasili Bandari ya Dar es Salaam kutoka nchini China Disemba 24, 2024.
Zoezi la ushushaji kutoka kwenye Meli litakapokamilika litafuatia zoezi la majaribio ambalo litajikita katika kutembeza mabehewa hayo kwenye Reli yakiwa tupu na kisha yakiwa yamebeba mizigo. Mabehewa hayo yatakuwa yanatembea kwa kasi ya kilometa 120 kwa saa.
Majaribio hayo yatakamilika mara tu wataalamu wa Shirika la Reli wakishirikiana na wale wa mkandarasi watakaporidhika kuwa utendaji kazi wa mabehewa hayo umekidhi viwango kulingana na Mkataba. Tarehe rasmi ya kuanza operesheni za mabehewa hayo, Shirika litauujulisha Umma.
Katika mabehewa hayo 264 yaliyowasili, 200 ni ya kubeba makasha (makontena) na mabehewa 64 ni ya kubeba mizigo isiyofungwa (loose cargoes).
Shehena hiyo ya mabehewa 264 ni sehemu ya jumla ya mabehewa 1,430 ambayo kwa mujibu wa mkataba yanatengenezwa na kampuni ya CRRC ya nchini China.
Novemba 15, 2024 Shirika liliutaarifu umma kuwa utengenezaji wa mabehewa 264 ya mizigo yatakayotumika katika reli ya kiwango cha kimataifa – SGR umekamilika nchini China na Meli iliyobeba mabehewa hayo iling’oa nanga katika Bandari ya Dalian, China Novemba 12, 2024.