TikTok imeita ripoti kwamba China inazingatia kuruhusu uuzaji wajukwaa la mtandao huo wa kijamii nchini Marekani kwa Elon Musk ni ” uongo mtupu.”
Maoni ya kampuni hiyo yanatolewa kujibu ripoti ya Bloomberg kwamba maafisa wa China wanazingatia chaguo ambalo linaweza kuhusisha biashara yake inayoendeshwa nchini Marekani kuuzwa kwa mtu tajiri zaidi duniani ikiwa Mahakama ya Juu Zaidi ya Marekani itadumisha marufuku dhidi ya mtandao huo.
Majaji wa Mahakama ya Juu Zaidi wanatakiwa kutoa uamuzi kuhusu sheria iliyoweka tarehe ya mwisho ya kuendesha mtandao huo wa TikTok kuwa Januari 19 ama kuuza uendeshaji wa shughuli zake nchini Marekani au ipigwe marufuku nchini humo.
TikTok imesema mara kwa mara kwamba haitauza uendeshaji wa shughuli zake nchini Marekani.
“Hatuwezi kutarajiwa kutoa maoni kuhusu kitu cha uwongo,” msemaji wa TikTok aliambia BBC News.
Bloomberg iliripoti, ikitoa mfano wa watu wanaofahamu suala hilo, kwamba hatua moja inayowezekana kufikiriwa kuchukuliwa na maafisa wa China ni jukwaa hilo la mtandao wa kijamii wa TikTok kuanza kuendeshwa na Musk ambaye anaendesha mtandao wa X.
Musk ni mshirika wa karibu wa rais mteule wa Marekani Donald Trump, ambaye anatazamiwa kurejea Ikulu ya White House tarehe 20 Januari.