Madiwani na viongozi wa Halmashauri ya Mji wa Nanyamba wamefanya ziara ya siku moja katika Jiji la Mwanza kwa lengo la kujifunza usimamizi wa miradi na mbinu za kuongeza mapato.
Ziara hiyo ni sehemu ya jitihada za kuboresha utendaji wa halmashauri hiyo iliyopo mkoani Mtwara.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Nanyamba, Mhandisi Mshamu Munde, amesema wamejifunza jinsi Mwanza inavyosimamia miradi ya maendeleo, ukusanyaji wa mapato, na utunzaji wa mazingira. Amebainisha kuwa lengo lao ni kuhakikisha wanatumia maarifa hayo kuboresha miradi yao na kufikia lengo la kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 3.5 mwaka ujao wa fedha.
Katika ziara hiyo, walitembelea dampo la Buhongwa, kiwanda cha matofali kinachosimamiwa na halmashauri, pamoja na Stendi Kuu ya Nyegezi. Viongozi hao wamevutiwa na namna miradi hiyo inavyoendeshwa kwa ufanisi na kutoa manufaa kwa jamii.
Aidha, Kaimu Mkuu wa Usafi na Mazingira wa Jiji la Mwanza, Desderius Pole, amewataka viongozi wa Nanyamba kuwekeza zaidi katika vyanzo vya mapato na kuendeleza miradi ya kimkakati ili kufanikisha malengo yao ya maendeleo.
Madiwani hao wamesema wanatarajia kutumia maarifa hayo kuboresha miradi kama ujenzi wa soko, dampo, na stendi, pamoja na kukuza vivutio vya utalii Nanyamba. Wameahidi kuleta mabadiliko chanya kwa kutumia uzoefu walioupata Mwanza.