Maelfu ya watu walikusanyika katika Msikiti wa Imam Muhammad bin Abdul al-Wahhab katika mji mkuu wa Qatar, Doha, kwa ajili ya sala ya mazishi ya kiongozi wa kisiasa wa Hamas Ismail Haniyeh.
Mzee huyo mwenye umri wa miaka 62 aliuawa nchini Iran pamoja na mlinzi wake siku ya Jumatano katika kile kundi la Palestina lilichokiita “uvamizi wa kihaini wa Wazayuni”. Israel haijathibitisha wala kukanusha kuhusika kwake.
Huku kukiwa na ulinzi mkali, waombolezaji walikusanyika katika boma la msikiti wa kitaifa saa chache kabla ya sala ya Ijumaa ya adhuhuri kuanza kutoa heshima zao kwa Haniyeh, ambaye aliishi Doha kwa miaka kadhaa iliyopita.
Alikuwa mwanachama mashuhuri wa vuguvugu hilo kwa zaidi ya miaka 20. Urithi wake katika mapambano ya Wapalestina ya kuwa taifa na uhuru kutoka kwa uvamizi wa Israel haukuweza kupingwa, kwa mujibu wa wengi waliokuwa kwenye msikiti huo.
“Israel imeua karibu Wapalestina 40,000 katika siku 300 zilizopita. Haniy alikuwa mmoja wao. Tutakumbuka kila maisha ambayo yalikatishwa na mauaji haya ya kimbari,” alisema Ahmed, Mpalestina anayeishi Doha.
“Tutapinga na tutaishi kuona Palestina huru,” aliongeza.