Mvua zinazoendelea kunyesha nchini Chad tangu mwezi Julai zimesababisha vifo vya watu 503 na kuathiri zaidi ya watu milioni 1.7, kwa mujibu wa ripoti iliyotumwa kwa shirika la habari la AFP siku ya Jumamosi na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) nchini Chad.
Kwa mujibu wa ripoti hii mpya “wilaya 117 kati ya 125 zimeathirika” ambapo nyumba 212,111 na heka 357,832 za mashamba zilihzribiwa. Na ng’ombe 69,659 zimesombwa na maji. “Mvua hizi zimesababisha mafuriko makubwa ambayo yameathiri majimbo yote ya nchi, na kusababisha watu kadhaa kupoteza maisha lakini pia uharibifu mkubwa wa nyenzo na mifugo,” alisema Marcelin Kanabé Passalé, Waziri wa Maji na Nishati wakati wa mkutano na waandishi wa habari siku ya Jumamosi asubuhi bila kutoa takwimu sahihi.
Waziri huyo pia alitangaza kuanzishwa kwa kamati ya ufuatiliaji wa mafuriko, ili “kutathmini hatari zinazohusishwa na uchafuzi wa vyanzo vya maji ya kunywa na kupanda kwa viwango vya mito”.
“Ilibainika kuwa maji ya Mto Logone na Mto Chari yamefikia kimo kikubwa ambacho kinaweza kusababisha mafuriko katika siku zijazo,” kulingana na waziri.
Umoja wa Mataifa ulionya mwanzoni mwa mwezi Septemba kuhusu athari za “mvua kubwa na mafuriko makubwa” katika kanda hiyo, hasa nchini Chad, ukitoa wito wa “hatua za haraka na ufadhili wa kutosha” kukabiliana na “mgogoro wa hali ya hewa”.