Jeshi la Chad limejeruhi na kuua wanachama wa kundi la Boko Haram katika mashambulizi ya anga, Rais Mahamat Idriss Deby Itno alisema siku ya Alhamisi.
“Tulifanya mashambulizi kadhaa ya anga kwenye maeneo ya adui ambayo yalisababisha vifo na kujeruhiwa kwa watu wengi,” Deby aliwaambia waandishi wa habari katika eneo la Ziwa Chad, bila kutoa idadi kamili.
Deby, ambaye alifanya mahojiano ndani ya magwanda ya kijeshi, alisema kuwa “binafsi” alianzisha shambulio la kukabiliana na Boko Haram, ambalo lilivamia jeshi la Chad katika shambulio la mwezi uliopita katika eneo la magharibi, karibu na mpaka na Nigeria.
Serikali ya Chad iliapa “kuwaangamiza” Boko Haram wakati ilipoanzisha operesheni yake, mwishoni mwa Oktoba baada ya wanamgambo hao kuua watu wapatao 40 na kujeruhi wengine katika uvamizi wa ngome ya kijeshi.