Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam imeikataa video ya maelezo ya mshtakiwa Miriam Mrita, mke wa aliyekuwa mfanyabiashara wa madini, Erasto Msuya ‘Bilionea Msuya’ kutokana na kukiuka matakwa ya kisheria.
Uamuzi huo umetolewa na Jaji Edwin Kakolaki anayeisikiliza kesi hiyo, baada ya kukubalina na hoja moja kati ya tano za pingamizi zilizoibuliwa na wakili wa mshtakiwa huyo, Peter Kibatala kuwa kielelezo hicho kilichokuwa kinaombwa kupokelewa mahakamani hapo hakikuwahi kuorodheshwa wala kusomwa katika hatia ya uhamishaji wa kesi hiyo kutoka Mahakama ya chini kwenda Mahakama Kuu, kama sheria inavyoelekeza.
Upande wa mashtaka katika kesi hiyo kupitia kwa shahidi wa sita, Mkaguzi wa Polisi (Inspekta), Alistides Kasigwa, kutoka Makao Makuu ya Jeshi ya Polisi, Kamisheni ya Uchunguzi wa Kisayansi, alieleza mahakama kuwa alimrekodi mshtakiwa huyo wakati akitoa maelezo yake akihojiwa na askari Inspekta Ratifa katika kituo kidogo cha Pilisi Uwanja wa Ndege, Dar es Salaam, Agosti 8, 2016.
Mbali na Miriam ambaye ni mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo namba 103 ya mwaka 2018, mshakiwa mwingine ni mfanyabiashara Revocatus Myella.
Wote wanakabiliwa na shtaka la mauaji ya kukusudia, wakidaiwa kumuua, mdogo wa marehemu Bilionea Msuya wa kike, Aneth Msuya nyumbani kwake, Kibada, Kigamboni jijjini Dar es Salaam, Mei 25, 2016