Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuhukumu kunyongwa hadi kufa, Mtanzania Dibron Said baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kumuua mkewe Herieth Justine kwa kumchoma na kisu begani, kifuani na tumboni baada ya kumfumania na mwanaume mwingine.
Akitoa hukumu hiyo leo Hakimu Mkazi Mkuu,Evodia Kyaruzi alisema mahakama imejiridhisha na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka wa mashahidi sita pamoja na ripoti ya kitabibu ya kifo cha marehemu, hivyo mahakama inamtia hatiani kwa kosa la kuua kwa kukusudia.
Kyaruzi alisema kutokana na ushahidi uliotolewa na mjomba wa marehemu,Castoly Salum jinsi alivyoshuhudia mshtakiwa huyo akimchoma kisu mkewe hadi umauti unamkuta pamoja na ripoti ya hospitali hivyo Mahakama hiyo inamuhukumu kunyongwa hadi kufa.
Katika kesi ya msingi, Said anadaiwa kutenda kosa lake Machi 11, 2018 katika eneo la Vingunguti ambapo anadaiwa kumuua kwa makusudi Herieth Justine, baada ya kumfumania akiwa na mwanaume mwingine.
Hata hivyo, inaelezwa kwamba mshtakiwa huyo baada ya kutekeleza mauaji hayo, alienda kituo cha Polisi Vingunguti na kabla hajaingia ndani alijichoma kisu tumboni hadi utumbo ukatokezea kwa nje akiwa na nia ya kujiua baada ya kumfumania mke akiwa na mwanaume mwingine ndani ya nyumba yake.