Leo February 27, 2020 Mahakama ya Hakimu Mkazi kisutu imekubali kupokea hoja za maombi ya mfanyabiashara James Rugemalira anayetaka kuondolewa kwenye kesi ya utakatishaji fedha wa Sh. Bil 309.4.
Hatua hiyo inakuja wakati shauri hilo lilipoitishwa kwa ajili y kutajwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi.
Wakili wa utetezi, John Chuma amedai kuwa mteja wake ameshawasilisha hoja za pingamizi la awali lakini hajapata majibu yoyote kutoka upande wa Jamuhuri.
Akijibu hoja hizo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon amedai baadhi ya nyaraka amezipata leo mahakamani hapo na kuwa upande wa Jamhuri upo tayari kusikiliza hoja hizo kwa njia ya mdomo kama nyaraka hizo zimeshaingizwa kwenye kumbukumbu ya mahakama hata kwa wakati huo kama ratiba ingeruhusu.
Wankyo amedai mshtakiwa wa pili amekua anajiwasilisha mwenyewe huku akiwa na uwakilishi wa mawakili hivyo anapaswa kusema kama amewaacha ama wanaendelea.
Akijibu suala hilo, Rugemarila amedai kuwa amekua na wawakilishi hata zaidi ya thelasini lakini kuna hoja lazima aziwasilishe mwenyewe na kuwa hilo jambo walitakiwa kulalamika mawakili wake na sio yeye kwani sheria inamruhusu kujiwakilisha.
Baada ya hoja hizo, Hakimu Shaidi Shaidi ameahirisha shauri hilo hadi Machi 12, 2020 litakuja kutajwa na upande wa jamuhuri kuwasilisha majibu.
Mbali na Rugemalira, washitakiwa wengine ni Mmiliki wa Kampuni ya Kufua Umeme ya Independent Power (IPTL) na Mwanasheria wa IPTL, Joseph Makandege.
Makandege anadaiwa kuwa, kati ya Oktoba 18, 2011 na Machi 19, 2014 katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam, Kenya, Afrika Kusini na India, akiwa na wenzake walikula njama ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Pia anadaiwa kuongoza genge la uhalifu, katika nchi hizo, akiwa si mtumishi wa Serikali akishirikiana na watumishi wa umma kwa kuratibu na kufadhili mpango wa uhalifu.
Katika mashitaka ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu Makandege anadaiwa kuwa kati ya Januari 23, 2014 na Februari 2014, alijipatia dola 380,000 katika benki ya Stanbic iliyopo Kinondoni na dola 600,000 katika benki ya UBL Bank(T) Ltd iliyopo wilaya ya Ilala, fedha zilizotoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa nyakati tofauti.
Washitakiwa Seth na Rugemalira kwa pamoja wanakabiliwa na mashitaka 12 yakiwemo ya utakatishaji fedha na kusababisha hasara ya Dola za Marekani 22,198,544.60 na Sh 309,461,300,158.27 kwa mara ya kwanza walifikishwa mahakamani hapo Juni 19, 2017.