Mahakama kuu ya Umoja wa Mataifa imefungua siku mbili za kusikilizwa kwa ombi la Afrika Kusini la kusitisha mashambulizi ya kijeshi ya Israel katika mji wa Rafah kusini mwa Gaza.
Ni mara ya nne Afrika Kusini kuitaka Mahakama ya Kimataifa ya Haki kuchukua hatua za dharura tangu taifa hilo lianzishe kesi inayodai kuwa hatua ya Israel huko Gaza ni sawa na mauaji ya halaiki.
Kulingana na ombi la hivi punde, amri za awali za mahakama yenye makao yake The Hague hazikutosha kushughulikia “shambulio la kikatili la kijeshi kwenye kimbilio pekee lililosalia la watu wa Gaza.”
Israel imeionyesha Rafah kama ngome ya mwisho ya kundi la wapiganaji wa Palestina Hamas, ikipuuzilia mbali maonyo kutoka kwa Marekani na washirika wengine kwamba mashambulizi yoyote makubwa huko yatakuwa janga kwa raia.
Afrika Kusini imeomba mahakama iamuru Israel ijiondoe Rafah; kuchukua hatua za kuhakikisha ufikiaji usiozuiliwa kwa maafisa wa Umoja wa Mataifa, mashirika ya kibinadamu na waandishi wa habari Gaza; na kuripoti ndani ya wiki moja jinsi inavyokidhi matakwa haya