Mahakama Kuu ya Zimbabwe imetoa hukumu iliyotupilia mbali ombi lililowasilishwa na wabunge 14 na maseneta tisa kutoka Chama cha upinzani cha Citizens’s Coalition for Change (CCC) wakitaka kurejeshewa nyadhifa zao ndani ya mabaraza hayo ya kutunga sheria.
Wanasiasa hawa wa upinzani ni wale walipokonywa nyadhifa zao za ubunge na useneta mwezi uliopita.
Wabunge na maseneta hao wamepoteza nafasi zao baada ya Sengezo Tshabangu, ambaye anadai kuwa ndiye katibu mkuu wa muda wa chama hicho cha upinzani CCC, kumtumia barua Spika wa Bunge la Zimbabwe, Jacob Mudenda tarehe 3 mwezi uliopita wa Oktoba, akidai kuwa wabunge hao si wanachama tena wa chama cha CCC.
Kauli hii ilipelekea kufukuzwa bungeni wanasiasa hao wa upinzani, licha ya maandamano ya kupinga pamoja na upinzani uliooneshwa na mkuu wa chama hicho, Nelson Chamisa. Wanachama na viongozi wengi wa chama cha CCC wanasema Sengezo Shabangu si kiongozi halali wa chama hicho na kwamba barua yake kwa Spika wa bunge haina itibari yoyote.