Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita (ICC) imetoa hati ya kukamatwa kwa Rais wa Urusi Vladimir Putin ikidai kuwa anahusika na uhalifu wa kivita, ikiwa ni pamoja na kuwahamisha Watoto kutoka Ukraine na kuwapeleka Urusi kinyume cha Sheria.
ICC imesema uhalifu huo ulifanyika Ukraine kuanzia February 24, 2022 wakati Urusi ilipoicamia Ukraine rasmi licha ya kwamba mara kadhaa Urusi imekanusha madai ya uhalifu wa kivita wakati wa uvamizi huo.
Kamishna wa Haki za Watoto wa Urusi, Maria Alekseevna Lvova-Belova, pia ni miongoni mwa wanaotakiwa kukamatwa kwa amri ya Mahakama ya ICC.
Licha ya kibali hicho cha kumkamata Putin na Bi Lvova-Belova kutolewa, ICC haina Mamlaka ya kuwakamata Putin na wenzake, na inaweza tu kutumia Mamlaka ndani ya nchi ambazo zimesaini makubaliano yaliyounda Mahakama hiyo, Urusi sio Mwanachama wa makubaliano hayo kwahivyo hakuna uwezekano wa Kiongozi huyo kuwasilishwa mbele ya Mahakama hiyo hata hivyo inaweza kuwanyima uhuru wa kusafiri.