Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC, imetoa siku ya Alhamisi, Novemba 21, hati ya kukamatwa kwa Benjamin Netanyahu na Waziri wake wa zamani wa Ulinzi Yoav Gallant kwa “uhalifu dhidi ya ubinadamu na uhalifu wa kivita”.
Hati ya kukamatwa pia imetolewa kwa mkuu wa tawi la kijeshi la Hamas Mohammed Deif
“Chumba kimetoa hati za kukamatwa kwa watu wawili, Bw. Benjamin Netanyahu na Bw. Yoav Gallant, kwa uhalifu dhidi ya ubinadamu na uhalifu wa kivita uliofanywa kuanzia angalau Oktoba 8, 2023 hadi Mei 20, 2024, siku ambayo upande wa mashtaka uliwasilisha maombi hayo kwa hati za kukamatwa,” ICC, iliyoko Hague, imesema katika taarifa yake, na kuongeza katika taarifa nyingine kwamba hati pia imetolewa dhidi ya Mohammed Deif.
Hati za kukamatwa ziliainishwa kama “siri”, ili kulinda mashahidi na kuhakikisha uchunguzi unaweza kufanywa, mahakama imesema.
Lakini “chumba kinaona kuwa ni kwa manufaa ya waathiriwa na familia zao kwamba wanafahamishwa kuhusu kuwepo kwa hati hizo,” imeeleza.