Mahakama moja ya Korea Kusini imetupilia mbali ombi linalopinga kuwekwa kizuizini kwa Rais anayeshutumiwa Yoon Suk-yeol na timu ya pamoja ya mamlaka za upelelezi.
Uamuzi huo wa jana Alhamisi wa Mahakama Kuu ya Eneo la Seoul ulifikiwa baada ya wanasheria wa Yoon, wanaosema kuzuiliwa kwake ni batili, kuwasilisha maombi ya kutaka mapitio ya uhalali wa kuzuiliwa huko, juzi Jumatano.
Yoon aliwekwa kizuizini na timu ya pamoja ya upelelezi juzi Jumatano akituhumiwa kwa makosa ya uasi kuhusiana na amri yake iliyodumu kwa muda mfupi ya sheria ya kijeshi, mwezi uliopita.
Yoon alikataa kutoa matamko wakati wa mahojiano na wapelelezi kabla ya kuhamishiwa katika kituo cha kizuizi nje kidogo ya mji wa Seoul. Aliendelea kupinga kuhojiwa jana Alhamisi, akisema tayari alikuwa ameleezea msimamo wake kikamilifu.
Vyombo vya habari vya Korea Kusini vinasema kwamba timu ya upelelezi inatarajiwa leo Ijumaa kuomba kibali cha mahakama cha kumkamata Yoon kwa upelelezi zaidi.