Mahakama ya Juu ya Venezuela, ambayo waangalizi wanasema ni mtiifu kwa serikali ya Rais Nicolas Maduro, siku ya Alhamisi ilimtangaza mshindi wa uchaguzi wa Julai 28 uliozozaniwa, huku kukiwa na madai ya upinzani ya kuenea kwa wizi wa kura.
Katika uamuzi wake uliosomwa na jaji msimamizi Caryslia Rodriguez, mahakama hiyo ilisema “imeidhinisha bila shaka nyenzo za uchaguzi na imethibitisha matokeo ya uchaguzi wa urais wa Julai 28, 2024 yaliyotolewa na Baraza la Taifa la Uchaguzi (CNE),” ikimtaja Maduro kuwa mshindi.
Maduro mwenyewe aliiomba mahakama mapema mwezi huu kutathmini uchaguzi huo, ambapo anadai kuwa alimshinda mgombea wa upinzani Edmundo Gonzalez Urrutia kwa asilimia 52 ya kura zilizopigwa, kulingana na CNE.