Ndugu wawili kutoka huko Singapore wamepelekana Mahakamani baada ya Kaka Kumshtaki Dada yake kwa kuingia chumbani kwake mara kwa mara kwa miaka minane ili kusafisha, jambo alilosema linavunja faragha yake na kumsababishia msongo wa mawazo.
Mahakama ya Familia huko Singapore imetoa amri za ulinzi kwa pande zote mbili baada ya Dada huyo kueleza kuwa kitendo chake kilitokana na dhamira ya kufanya usafi kutokana na hali ya Chumba cha Kaka yake ingawaje, Kaka huyo alidai kitendo hicho kimekuwa kikivuruga utulivu wake na kumfanya alazwe katika Taasisi ya Afya ya Akili mara kadhaa.
Baada ya ugomvi kuibuka juu ya suala hilo, Dada huyo aliomba amri ya ulinzi akidai kushambuliwa na Kaka yake kutokana na mvutano uliosababishwa na suala la usafi, Jaji Tan Zhi Xiang kutokea Mahakama hiyo ya Familia alisema kuwa, kwa mujibu wa sheria, vitendo vya Dada huyo vinaweza kuchukuliwa kama usumbufu wa kimakusudi na vinachukuliwa kama unyanyasaji wa kifamilia.
Mahakama ilikubali kuwa kuingia Chumbani kwa Mtu bila ruhusa hasa usiku kunaweza kuwa chanzo cha kero na kuvuruga utulivu, na kwamba Kaka alikuwa ametoa malalamiko mara kadhaa kuhusu hilo hata hivyo Dada huyo alijitetea kuwa ratiba yake ya kazi humlazimu kufanya usafi wakati huo, akieleza kuwa hakuwa na wakati mwingine wa kufanikisha hilo.
Jaji alihitimisha kuwa, ingawa usafi ni muhimu, haikustahili Dada kulazimisha kwa kaka yake na Mahakama iliamuru amri za ulinzi kwa pande zote, ambapo Dada amezuiwa kuingia Chumbani kwa Kaka na Kaka amepewa amri ya kutomshambulia Dada yake.