Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemuagiza kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa {TAKUKURU} Mkoa wa Katavi awachunguze watumishi wawili akiwemo Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Mazingira Mpanda {MUWASA}, Hussein Nyemba kwa tuhuma za kukiuka taratibu za manunuzi ya Umma.
Mwingine ni Afisa Mipango Miji wa Halmashauri ya wilaya ya Tanganyika Bw Abraham Casto ambaye anadaiwa kujipatia ardhi katika vijiji mbalimbali bila ya kufuata taratibu za kisheria na kusababisha migogo ya ardhi baina yake na wanavijiji.
Watumishi wote hao wawili wamesimamishwa kazi kupisha Uchunguzi wa tuhuma zinazowakabili.
Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo alipozungumza na watumishi wa Halmashauri za Mpanda, Nsimbo na Tanganyika katika ukumbi wa Mpanda Social Hall akiwa katika ziara ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa mkoani Katavi.
Pia Waziri Mkuu ameiagiza TAKUKURU ichunguze ununuzi wa pikipiki 30 zilizonunuliwa Jijini Dar es Salaam kwa gharama ya sh. milioni 3.8 kila moja huku wilayani Mpanda pikipiki moja inauzwa sh. milioni 2.7, pia ununuzi wa mita za maji 1,000 uliofanywa bila ya kukaguliwa na TBS pamoja na ajira ya watumishi 25 alizoajiri bila kibali.