Mgawanyiko unaoongezeka kati ya familia mbili zenye nguvu zaidi za kisiasa nchini Ufilipino ulidhihirika hadharani baada ya Makamu wa Rais wa taifa hilo la Kusini-mashariki mwa Asia Sara Duterte bintiye rais wa zamani Rodrigo Duterte kusema kwamba angefanya Rais Ferdinand Marcos Jr auawe ikiwa atauawa.
Sasa, mamlaka ya sheria na utaratibu nchini Ufilipino inachunguza vitisho vilivyotolewa na Makamu wao wa Rais, na Bi Duterte anaweza kufunguliwa mashtaka iwapo ushahidi utapatikana kuunga mkono dai lake.
“Vitisho vya Duterte sasa vinachunguzwa na huenda vikamfungulia mashtaka,” Ofisi ya Mawasiliano ya Rais ilisema, ikinukuu wizara ya sheria.
“Ikiwa ushahidi utakubali, hii inaweza kusababisha kufunguliwa mashitaka,” ofisi ya Bw Marcos ilisema kwenye taarifa.
Katibu Mtendaji Lucas Bersamin alirejelea “tishio kali” dhidi ya Rais Ferdinand Marcos Jr kwa kikosi cha walinzi wa rais “kwa hatua sahihi za haraka”.
Kamandi ya Usalama wa Rais mara moja iliimarisha usalama wa Marcos na kusema inazingatia tishio la makamu wa rais, ambalo “lilifanywa kwa ujinga sana hadharani”, na ni suala la usalama wa taifa kutekeleza sheria kugundua, kuzuia, na kutetea dhidi ya vitisho vyovyote kwa rais na familia ya yake”.
Mshauri wa Usalama wa Kitaifa Eduardo Ano pia alisema serikali inachukulia vitisho vyote kwa rais kuwa “vikubwa”, akiahidi kufanya kazi kwa karibu na vyombo vya sheria na ujasusi kuchunguza tishio hilo na wahusika wanaowezekana kukamatwa.
“Vitisho vyovyote dhidi ya maisha ya rais vitathibitishwa na kuchukuliwa kuwa suala la usalama wa taifa,” Bw Ano alisema kwenye taarifa.
Haijafahamika mara moja ni hatua gani zitachukuliwa dhidi ya makamu huyo wa rais.