Wawakilishi wa zaidi ya vyama 180 vya Kikatoliki na Kiinjili walifanya maandamano Alhamisi katika mji mkuu wa Uhispania kupinga vita vya Israel dhidi ya Gaza.
Walikusanyika mbele ya ubalozi wa Israel mjini Madrid kwa mshikamano na Wapalestina katika Ukanda wa Gaza.
Wakiimba nara za Wapalestina, wanachama wa umati huo walishikilia mabango ya kusema “Palestina Huru” na “Haki.”
Akizungumza na vyombo vya habari, Padre wa Kanisa Katoliki Nicase Theron alisema walihudhuria maandamano hayo ya kutaka amani na kuonyesha uungaji mkono wao kwa Wapalestina ambao wamekuwa wakiteseka kwa muda mrefu.
“Komesha mauaji haya kwa jina la ubinadamu,” Theron alisema.
Mandamanaji mwingine, Margarita Jimenez, aliikosoa Israel kwa kushambulia Ukanda wa Gaza, akisema majeshi ya Israel yanaua wanawake na watoto, yanashambulia kwa mabomu hospitali na kutoruhusu misaada ya kibinadamu kuingia.
Akizungumzia maazimio ya Umoja wa Mataifa kuhusu suluhu ya mataifa mawili, Jimenez alibainisha kuwa Israel haijawahi kuyatambua na inajaribu kuwafukuza Wapalestina katika ardhi yao.