Malawi itaanza kuagiza unga wa mahindi kutoka Tanzania na Afrika Kusini ili kulisha watu wake milioni 4.4 wanaokabiliwa na uhaba wa chakula nchini humo.
Kamishna wa Idara ya Masuala ya Kukabiliana na Maafa ya Malawi (DoDMA) Bw. Charles Kalemba amewaambia hayo wanahabari mjini Lilongwe, kwenye mkutano kati ya Rais Lazarus Chakwera na Mkurugenzi wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) wa Ofisi ya Kanda ya Kusini mwa Afrika, Bwana Menghestab Haile.
Kauli ya Bwana Kalemba imeondoa utata uliosababisha Malawi iache kuagiza mahindi kutoka Tanzania na Kenya kutokana ugonjwa wa mahindi uliotajwa na wataalam wa Malawi.
Hivi karibuni ripoti za vyombo vya habari vya Malawi zilionyesha kwamba Benki ya Dunia ilitoa dola za Kimarekani Milioni 20 kununua mahindi kutoka Tanzania ili kuwasaidia wamalawi wenye mahitaji, lakini ripoti zilisema Benki ya Dunia ilikwamishwa na marufuku ya uagizaji wa bidhaa hiyo.