Tuzo za Malkia wa Nguvu zinazoendeshwa na Clouds Media Group zimehitimishwa usiku wa Novemba 29 2024 Zanzibar kwa Malkia wa nguvu tisa kupewa tuzo kwenye sekta mbalimbali wanazohudumia.
Mbele ya Mgeni rasmi Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi, Mhandisi Zena Said amewataka Wanaume kwenye maeneo mbalimbali kuwapa ushirikiano Wake zao haswa wenye maono makubwa ya Kiuchumi na kijamii.
Washindi waliotangazwa ni pamoja na Ramla Khamis Juma, yeye ameshinda kwenye kipengele cha Biashara ya Chakula, ni mkazi wa Pemba, kwa sasa ni Mpishi mkubwa ambae alianza kupika akiwa mtaani mpaka baadae kuajiriwa Ikulu kama mpishi, lakini bado alikua na ndoto ya kusimamisha biashara yake mwenyewe, kwa sasa amefanikiwa kusimamisha biashara yake na ameajiri zaidi ya Wafanyakazi 200.
Mwingine ni Aisha Bakari Mohamed (Hijab Dj) yeye ameshinda tuzo ya Sekta ya Burudani, akiwa Binti mdogo aliyezua gumzo kwa kuonekana DJ anayepiga muziki bila kuonyesha maungo yake, yeye ni hijab mwanzo mwisho, Kwa sasa umaarufu wake si Zanzibar pekee ni mpaka nje ya Zanzibar anapata mialiko ya kwenda kupiga muziki.
Mshindi Mwingine ni Saida Abdallah Mohamed, aliyeshinda tuzo ya Sekta ya Viwanda kupitia biashara ya viungo mbalimbali vya Chakula, ameifanya kazi hii kwa miaka kumi sasa.
Sekta ya Ujasiriamali Bora Tuzo imeenda kwa watu wawili, Wa kwanza ni Fatma Eliah Masimba aliyeanza kuwa mhudumu wa Mapokezi wa Hotel baadae akawa mmiliki mwakilishi, kwa sasa yeye ni mkurugenzi katika biashara kubwa ya familia yake, akiwa Mfanyakazi wa hoteli alikutana na Mume wake, Safari ya ujasiriamali na bishara imeendelea wakiwa wawili na kwa sasa anasimimamia bishara mbalimbali ikiwa ni pamoja na vituo vya mafuta, ujenzi na usafirishaji.
Ujasiriamali tuzo nyingine imeenda kwa Fatma Salum Abdalah (Bi Sufa), yeye aliozeshwa akiwa na miaka 14 mara baada ya kuhitimu elimu ya msingi, baadae matokeo yalitoka akawa amefaulu hivyo akaendelea na masomo. Alipomaliza shule, alianza maisha yake ya ujasiriamali na bishara nyingi katikati ya changamoto. Kutokana na maisha yake kutopata msingi mzuri wa kusoma aliamua kuanzisha shule na kuziita Sufa Schools ambazo zipo kwa zaidi ya miongo miwili, mbali na shule ni mmiliki wa store kubwa ya vitu vya jumla, frame za kupangisha na mkulima mkubwa kutokana na mashamba aliyonayo.
Tuzo sekta ya Ustawi wa Jamii imeenda kwa WANU HAFIDH AMEIR, yeye ni mwanzilishi wa Taasisi ya Mwanamke Initiatives Foundation, Kupitia Mwanamke Initiatives Foundation, Wanu ameweka alama isiyofutika Kwa kujali afya za wanawake, taasisi hii imeboresha huduma za afya ya uzazi na akili sambamba na kutoa mafunzo muhimu kwa wahudumu wa afya wa jamii. Kwa vijana, ameongoza njia mpya kwa kuwapa nafasi za mafunzo ya kiufundi na teknolojia.
Sekta ya Mitindo na Urembo mshindi ni
Tatu Suleiman, Yeye ameamua kuongeza thamani ya zao la mwani kwa kutengeneza vipodozi asili. Ni mwanzilishi wa bidhaa za Zaidat ambapo amefanikiwa kushika soko la ndani na nje ya Zanzibar.
Sekta ya Utalii, Mshindi ni Mafunda Kombo Faki ambae ni mwanzilishi na mkurugenzi wa ZanVacay. Kupitia ZanVacay, sio tu kwenye eneo la utalii linalohitaji kuongezewa thamani, ZanVacay imemtambulisha Mafunda katika ulimwengu wa kukutana na vijana, kutoa mafunzo mablimbali yanayohusisha uongezaji wa thamani, pamoja na kuwa mmiliki wa ZanVacay, Mafunda pamoja na kuwa Mkurugenzi lakini ni mwajiriwa katika shirika la bima, na ni mshereheshaji katika matukio mbalimbali.
Tuzo ya Heshima imeenda kwa Mama Mariam, Mke wa Rais wa Zanzibar, muanzilishi wa taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF).
ZMBF imewagisa Wanawake wanaojishughulisha na uchumi wa buluu kwa makundi na kuwapatia boti za kisasa zenye mashine, vifaa vya kazi, na tumaini jipya na kubadilisha taswira ya maosha yao.
Kupitia Maisha Bora, Afya Bora, maelfu ya watu – wanawake, watoto, na wazee – wamepata huduma za vipimo na matibabu kutoka kwa madaktari bingwa. Zaidi ya watu 10, 000. mengine yaliyofanywa na taasisi hii ni pamoja na maswala ya Lishe, elimu jumuishi katika maswala ya ki uchumi, afya na masuala ya unyanyasaji wa kijinsia.