Vita kati ya majenerali wa Sudan vinazidi kuwa na madhara makubwa kwa raia, wiki hii idadi ya watu waliolazimika kuyahama makazi yao imeongeza maradufu, Umoja wa Mataifa ulisema siku ya Jumanne.
Tayari mamia ya watu wameuawa kutokana na mapigano hayo, lakini wasiwasi mpya umeibuka wakati mapigano tofauti ya kikabila yakiwa yameua watu 16 katika eneo la kusini mwa nchi, kundi lenye nguvu liloloko mashariki, eneo ambalo hadi sasa halijaathiriwa na vita, linaonyesha kuliunga mkono jeshi.
Hadi sasa zaidi ya watu 700,000 wamekoseshwa makazi ndani ya nchi kutokana na mapigano ambayo yamekuwa yakiendelea kwa wiki ya nne, Paul Dillon, msemaji wa Shirika la Kimataifa la Uhamiaji, alisema mjini Geneva.
Na kuongeza kuwa idadi hiyo imeongezeka maradufu katika kipindi cha wiki moja.
Sudan imejikuta kwenye machafuko wakati mapigano yalipozuka Aprili 15 kati ya vikosi vya mkuu wa jeshi Abdel Fattah al-Burhan na naibu wake aliyegeuka kuwa hasimu Mohamed Hamdan Daglo, anayeongoza kikosi cha Rapid Support Forces (RSF). Watu takriban 750 wamekufa.
Hata kabla ya mapigano kuanza, watu milioni 3.7 waliandkishwa ni wasiokuwa na makazi ndani ya nchi, aliongeza Dillon.
Watu wengine 150,000 wameikimbia nchi hiyo tangu mzozo huo ulipoanza, kwa mujibu wa idadi iliyotolewa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi siku ya Jumatatu.
Mazungumzo ya hivi karibuni ya kusitisha mapigano huko Saudi Arabia hayakuzaa matunda, huku mwanadiplomasia wa Saudia akisema pande zote mbili zinajiona “kuwa na uwezo wa kushinda vita”.
Shirika la habari la Reuters limeripoti kuwa wafanyakazi wa misaada wamesema mapigano kati ya makundi hasimu ya kijeshi nchini Sudan yanakandamiza programu za huduma za kibinadamu zenye ufadhili duni katika kanda hiyo kufikia hatua ya kushindwa kufanya kazi.
Hata kabla ya ghasia kuanza tarehe 15 Aprili, mamilioni Ya Wasudan na nchi jirani walikuwa wakitegemea misaada kutokana na umaskini pamoja na migogoro. Tangu vita ianze mamia ya watu wameuwawa, wakiwemo wafanyakazi wasiopungua watano wa mashirika ya kutoa huduma za kibinaadamu; na kupora akiba ya chakula; na wafanyakazi wengi wa kimataifa wa misaada wameondoka.
Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR linatafuta nyongeza ya dola millioni 445 ili kukabiliana na msafara mkubwa wa watu 860,000 unaotarajiwa kwenda nchi sita kati ya nchi saba jirani na Sudan – Chad, Misri, Ethiopia, Eritrea, Sudan Kusini na Jamhuri ya Afrika ya Kati – ifikapo Oktoba.
Kabla ya vita kuzuka tarehe 15 Aprili, watu takriban milioni 16 walikuwa wakitegemea misaada ya kibinadamu. Kulingana na Makadirio ya ndani ya Umoja wa Mataifa ambayo shirila la habari la Reuters imeyapata.